Mhandisi wa Mawasiliano wa TCRA, Mwesigwa Felician, alitaja hatua ya kwanza ya kuhama mtandao mmoja wa simu kwenda mwingine kuwa ni kufika kituo cha mauzo au kwa wakala anayetambuliwa na mtoa huduma anakotaka kuhamia na kumueleza dhumuni lake.
Hatua ya pili, alisema Felician, ni kujaza fomu maalum ya maombi ya kuhamia mtandao aliotaka kuhamia.
Felician alitaja hatua ya tatu kuwa ni kujaza tamko la kukubali kuwa mteja anakubali kuwajibika kwa madeni yoyote ambayo yanatokana na huduma alizokuwa akipata kwa mtoa huduma wa awali kama yatakuwapo.
Felician alitaja hatua ya nne ni kuwa ni kuwasilisha kitambulisho chenye picha ambacho kinaweza kuwa cha taifa, kadi ya mpiga kura, leseni ya udereva, pasipoti au kitambulisho chochote rasmi kinachotambulika.
Alisema pia mteja anatakiwa kuwa na simu ya kiganjani inayofanya kazi yenye namba inayotakiwa kubaki baada ya kuhama mtandao.
Hatua ya tano, Felician alisema ni kuhamisha fedha zilizopo kwenye akaunti ya simu kabla ya kuhama ili kuepuka usumbufu.
Katika hatua ya sita, Felician alisema, mwenye namba ya simu atatakiwa kutuma ujumbe mfupi wa maneno wenye neno HAMA kwenda namba 15080 ambayo ni namba maalum ya kuhama.
Alisema katika hatua ya saba, mteja atapokea ujumbe mfupi wa maneno utakaomjulisha kuwa ombi lake limekubaliwa.
“Hatua ya nane, iwapo namba yako haikuzuiliwa au kusimamishwa kwa muda kutokana na kutokamilisha malipo ya madeni ya mtoa huduma wako wa awali, maombi yako yatashughulikiwa na utajulishwa kwa ujumbe mfupi wa maneno maendeleo ya mchakato huo,” alisema Felician.
KAMA KAWAIDA
Alisema katika hatua ya tisa, mtoa huduma za simu za kiganjani atampatia mteja wake mpya laini mpya ya simu.
Hatua ya 10, Felician alisema, ni kusitishwa kwa huduma za kifedha kwa muda mpaka namba ya mteja itakapohamishwa kwa mtoa huduma mpya. Kuanzia hapo mwenye namba atatumia huduma za kifedha za mtandao mpya kama huduma zipo.
Mhandisi wa Mawasiliano wa TCRA Felician alisema katika hatua ya 11, huduma za kupiga na kupokea simu na ujumbe mfupi wa maneno zitaendelea kama kawaida.
Alisema katika hatua ya 12, mteja atakuwa amehama mtandao mmoja kwenda mwingine na kama patakuwa na ucheleweshaji, ni wa saa kadhaa, lakini ndani ya siku mbili pekee.
“Wakati huo namba yako ya zamani itakuwa imehamishwa kwa mtoa huduma wako mpya na laini yako ya awali haitatumika tena na utapokea ujumbe mfupi wa maneno kuwa uhamaji umekamilika,” alisisitiza Felician.
Katika hatua ya 13, mteja atatakiwa kuweka laini yake aliyopewa kwenye simu na endapo elimu zaidi itahitajika, mteja atatakiwa kwenda kwa mtoa huduma kujua namna ya kutumia huduma hiyo mpya.
MASHARTI NA VIGEZO
Mbali na kuelezea hatua hizo za kujiunga, Felician alisema masharti na vigezo vitavingatiwa ambavyo alivitaja kuwa ni mteja kutoweza kuhama na namba iliyofungiwa au kusitishiwa huduma kwa walipaji wa kabla ya huduma.
Alisema pia mteja hataweza kuhama na salio lililopo na atatakiwa kutumia salio lake kwanza kabla ya kuhama kwani vinginevyo, litapotea.
Pia alisema mteja hataweza kuhama iwapo ana mkopo kutoka kwa mtoa huduma wa awali, mikopo mingine kwa njia ya muda wa maongezi na pesa mtandao.
Felician alisema pia mteja hataweza kuhama iwapo namba yake inahusishwa na uhalifu na imefungiwa.
Kwa wateja wanaotumia utaratibu wa malipo baada ya kutumia huduma, watatakiwa kulipa madeni ya matumizi yao kabla ya kuhama, alisema.
Wateja hao, watatakiwa pia kukamilisha masharti ya mkataba ya mtoa huduma wake na kutizama masharti ya malipo kila mwezi kwa mujibu wa mkataba kabla ya kuhama, alisema zaidi Felician.
Alisema pia wataendelea kupokea ankara za matumizi hadi namba itakapohamishiwa kwa mtoa huduma mpya.
“Utaendelea kupokea ankara ya mwisho hadi siku 60 baada ya kuhamisha namba yako," alisema Felician.
"Utapewa mpaka siku 30 za kulipa ankara hizo, vinginevyo utakuwa katika hatari ya uhamaji wako kusitishwa au namba yako kufungiwa.”
Awali akizundua huduma hiyo, Mhandisi Kilaba alisema ili kufahamu mtumiaji wa simu unayempigia amehama mtandao “utasikia milio miwili kabla ya simu kuita."
"Hii milio ndiyo ambayo watu waliokuwa wanasema TCRA tumeanza kusikiliza mazungumzo ya watu, naomba muwaeleweshe Watanzania.”
Alisema kwa sasa kuna laini za simu milioni 40.1 nchini na kwamba lengo la kuleta huduma hiyo ni kuboresha na kupanua huduma za mawasiliano nchini.