Audio Mp3

audio song

Thursday, May 31, 2018

UKAWA wapigwa chenga

BUNGE jana 'liliupiga chenga ya mwili' Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) baada ya kupitisha makadirio ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.....

.....kwa mwaka ujao wa fedha bila uwapo wa mbunge hata mmoja wa upande huo, ikiwamo chama kikuu cha upinzani nchini Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Katika kikao cha jana cha Bunge kilichofanyika kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa saba mchana, hapakuwa na mbunge hata mmoja wa Chadema bungeni kutokana na kile kilichoelezwa na uongozi wa chama hicho kuwa wabunge wake wengi walikuwa mkoani Kigoma kushiriki mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Buyungu, Kuasuku Bilago.

Mwili wa mbunge huyo aliyefariki dunia Jumamosi kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) uliagwa juzi na wabunge jijini Dodoma kabla ya kusafirishwa kwenda Kigoma kwa ajili ya mazishi.

Huku ratiba ya vikao vya Bunge la Bajeti ikionyesha makadirio ya bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi yalipaswa kujadiliwa kwa siku tatu, Bunge jana lilitumia muda wa takribani saa nne kuyajadili na kuyapitisha huku viti vinavyokaliwa na wabunge wa Chadema vikiwa tupu.

Ratiba ya vikao vya Bunge la Bajeti inaonyesha kuwa makadirio ya bajeti ya wizara hiyo yalipaswa kujadiliwa bungeni kwa siku tatu kuanzia Jumatatu, lakini hayakuwasilishwa bungeni siku hiyo kutokana na Naibu Spika Dk. Tulia Ackson kutangaza kuahirisha shughuli za Bunge kufuatia kifo cha Bilago.

Juzi, Waziri wa wizara hiyo, William Lukuvi, aliwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake lakini hayakujadiliwa na Bunge kwa kuwa kulikuwa na shughuli ya kuaga mwili wa Bilango kwenye Viwanja vya Bunge.

Wakati wa kuipitisha bajeti hiyo jana, hakuna mbunge hata mmoja wa vyama vilivyokuwa na wabunge bungeni jana aliyewasilisha hoja ya kuzuia mshahara wa waziri, hivyo bajeti hiyo ya Sh. bilioni 65 kupita bila kupingwa.

Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu, aliyekuwa anaongoza kikao hicho, alisema kukosekana kwa mbunge wa kuipinga bajeti hiyo ni matokeo ya uchapakazi wa Waziri Lukuvi na wasaidizi wake.

Bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha (2017/18) pia ilipita bila kupingwa na mbunge yeyote wakati wa Bunge la Bajeti la mwaka jana huku Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, akiwataka mawaziri wengine kuiga utendaji wa Lukuvi.

'TUPO KIGOMA'

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika, alipotafutwa kuzungumzia kutokuwapo kwa wabunge wote wa chama chake bungeni jana alisema: "Kimsingi wabunge wengi tupo huku Kigoma na wachache wana udhuru."

Mbunge wa Kibamba huyo alibainisha kuwa wabunge wa chama chake watarejea bungeni kushiriki vikao vya Bunge baada ya mazishi.

No comments:

Post a Comment