BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI
(NACTE)
TAARIFA
 KWA UMMA KUHUSU UDAHILI WA WANAFUNZI WA ASTASHAHADA NA STASHAHADA 
KATIKA PROGRAMU MBALIMBALI KWA MWAKA WA MASOMO 2017/2018
Baraza la
 Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ni chombo kilichoanzishwa kwa sheria 
ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi, Sura 129, ili kusimamia na 
kuratibu utoaji wa mafunzo ya elimu ya ufundi nchini. Sheria hii 
inazitaka Taasisi zote zinazotoa elimu ya ufundi kusajiliwa kabla ya 
kuanza kuendesha mafunzo yoyote. Baraza pia huidhinisha mitaala kabla 
haijaanza kutumika. Hivyo taasisi zote haziruhusiwi kuanza kutoa mafunzo
 yoyote bila kibali maalumu kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi 
(NACTE).
Baraza linapenda kuwataarifu wadau wa sekta ya Mafunzo ya Ufundi na Umma kwa ujumla kuwa udahili na uchaguzi wa wanafunzi kwa ajili ya masomo ya Astashahada na Stashahada mbalimbali yanayotolewa na vyuo vyote hapa nchini, utafanyika moja kwa moja vyuoni,
 isipokuwa kozi za afya na ualimu zinazotolewa na  vyuo vya Serikali tu.
 Hivyo maombi yote ya nafasi za masomo yatumwe kwenye chuo husika.
 Udahili 
wa kozi za Afya na Ualimu katika vyuo vya Serikali  utaratibiwa na 
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto; na Wizara 
ya Elimu, Sayansi na Tekinolojia kwa kushirikiana na Baraza (NACTE). 
Hivyo maombi ya Udahili kwa kozi za Afya na Ualimu kwa vyuo vya serikali tu yatumwe kwa njia ya mtandao kupitia tovuti ya NACTE (www.nacte.go.tz) au kupitia vyuo husika vya Afya na Ualimu ambavyo vitashughulikia maombi hayo na kufanya udahili kwa njia ya mtandao kupitia ‘Institutional Panel’ zao.
Aidha 
vyuo vyote vitatangaza au kuwafahamisha moja kwa moja waombaji majina ya
 watakaochaguliwa kujiunga na kozi mbalimbali; na wale wa kozi za Afya 
na Ualimu watatangazwa na Wizara husika na kupitia tovuti ya NACTE.
Baraza 
linapenda pia kuwafahamisha kuwa Vyuo vitaanza kupokea maombi ya udahili
 wa wanafunzi kuanzia tarehe 15 Mei, 2017 hadi tarehe 20 Agosti, 2017. 
Majina ya waliochaguliwa yatatangazwa tarehe 14 Septemba, 2017. Masomo 
kwa mwaka wa masomo 2017/2018 yanatarajiwa kuanza rasmi tarehe 25 
Septemba, 2017.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA KATIBU MTENDAJI 
BARAZA LA TAIFA LA ELIMU YA UFUNDI (NACTE)
TAREHE: 10/05/2017

No comments:
Post a Comment